Sunday, 19 July 2015

SARATANI INAYOUA MZIKI WA PWANI

Ni kwa siku nyingi saana mziki wa pwani umekua kaburini na unazidi kutapatapa kujitoa uonekane katika hatua za juu.Wengi wamejiuliza ni kipi kinachosababisha hali hii huku kukiwa na hali ya kurushiana lawama ila kulingana na upeo wangu mdogo wa mziki nilionao nahisi kwamba kila mshikadau kuanzia producer,watangazaji na ma DJ,wasanii wenyewe hadi mashabiki wote wamechangia katika hali hii.
MASHABIKI.
Labda nianze na shabiki,Ni kwa mda mrefu saana sasa msanii wa nyumbani amelalamika saana kwamba wewe shabiki unamnyima nafasi kwenye skio lako na kwamba nafasi hiyo umewapa wasanii wa magharibi mwa africa pamoja na marekani.Hii ni hali ambayo msanii wa pwani imezidi kumkatisha tama sana.Kufikia kiwango cha msanii Kaa La Moto kutunga wimbo uliokemea hali hii na kumhimiza kila mkenya kiujumla kuukumbatia na kuukubali mziki wa nyumbani kwanza kabla kuupa nafasi mziki wa mataifa mengine.Kwanza pongezi kwa msanii KAA LA MOTO kwa wimbo KLM IS DEAD,pili kwa tatizo hili lawama itaanguka popote pale iwe kwashabiki,presenters,DJS,Maproducer miongoni mwa washikadau wote katika sanaa. Anayebisha kuwa pwani hakuna vipaji ni muongo au kiufupi tuseme tu ana laana maana kwa upeo wangu mdogo wa muziki nilionao naweza kusimama mbele ya watu na kujivunia vipaji vya wasanii kama Ally BJohnny Skani,Dazlah Kiduche,Majid,Susumila,Amoury beyby,Dogo Richie,Kaa la Moto,Nyota Ndogo,Lovemums, Jovial,Kigoto Mmbonde,Alkenia Love,Shaah Biggy,Chikuzee,Shembwana Masauti,Fisherman,Canibal,Sharama,Mchafuzy, Sudi Boy, Lai miongoni mwa wasanii kibao tu ambao kila siku wanakesha wakijaribu kila wanaloliweza kutupatia kazi nzuri na kuuweka mziki wa pwani katika ramani ya kitaifa na kimataifa kiujumla.
Ninachoamini ni kuwa wasanii wetu japo sio wote bali wengi wao wana nia hivyo basi sisi kama mashabiki.Tukiwapa sapoti ni dhahiri kuwa itawapa moyo wa kufanya bidii kuimarisha sanaa hii na kufikia viwango vya kupendeza kila skio.Sijasema kuwa ususie kazi nzuri za wanamziki wa inje ya pwani,  hapana....ninachomaanisha ni kuwa tusiwe watumwa wa kiakili kupenda zaidi vya wenzetu kufikia kiwango cha kudharau kazi nzuri za wasanii wa hapa kwetu.
Nafasi iko kubwa ya kuimarisha uchumi wa sanaa yetu ya nyumbani na kabla nizungumzie fursa hizo kwanza kila shabiki anafaa kutambua kuwa sanaa ya kila msanii iko kwa mikono ya yeye shabiki,hivyo ina maana kubwa kuwa msanii hata awe na bidii kiasi gani bila shabiki ni dhahiri atafeli tu,maana katika kila kazi anayotoa msanii,ni lazima shabiki apate kuiskia,aipende na aipitishe moyoni mwake.Pia tunafaa kuelewa kuwa kumkubali na kumsifia msanii pekee hakutamuekea chakula mezani wala kumuimarisha kisanaa,shabiki anachofaa kutambua ni kwamba sanaa ni kazi wala sio ngazi ya kutengeneza maskini wenye umaarufu.Hivyo basi ni utovu mkubwa wa shukrani,unafik na kukosa uzalendo kama shabiki hatampa sapoti msanii wa nyumbani na kuhamisha sapoti hiyo kwa wasanii wa kigeni.Hapo ndio tunarudi tena katika zile fursa za kuukuza uchumi wa soko letu la mziki ambazo nimekudokezea hapo awali.
Naam,shabiki unafaa kutambua kuwa kwa kununua kazi za msanii,iwe ni kwa mfumo wa ulbum au mifumo ya kidijitali kama vilemkito,mdundo, miito ya simu pamoja na mifumo yote ya mitandao kunampa mapato makubwa saana msanii.Pia wewe kama shabiki ukijitahidi kuhudhuria matamasha ya wasanii wa nyumbani ni kitu kinachompa nguvu sana msanii na kumtengenezea maslahi yanayomuongezea mbolea katika safari yake ya mziki maana ni kupitia mapato haya ndio watajibidisha hata kujitangaza nnje ya pwani kupitia bidii ya kutoa mziki mzuri na video zilizo na ubora wa kimataifa.

MAPRESENTER NA MA DJ 
Hawa ni washikadau wawili ambao ni nguzo kubwa saana katika mziki maana ndio wanaotegemewa na msanii kufikisha kazi kwa mashabiki na pia vilevile shabiki amewekeza uaminifu wake kwa wawili hawa kujua kwamba akihitaji mziki mzuri atakua anaupata kila siku kupitia kwao.Sanaa ikidondondokea pua lawama kubwa itawaendea wawili hawa,endapo sanaa itaimarika basi ni wazi kuwa asilimia kubwa ya sifa itawarudia wawili hawa.Naheshimu saana juhudi za DJs na PRESENTERS ila ujumbe unaofaa kuwaendea ni kwamba mziki m'bovu ni m'bovu tu hata uchezwe mara milioni kwa siku.Hakuna kitu kibaya kama kuona mziki unadidimia kila siku wakati mziki mzuri unanyimwa nafasi hewani huku mziki m'bovu ukipewa nafasi kisa upendeleo au mtu hongo.Ni picha ya kusikitisha kuona chat za top ten zikitawaliwa na nyimbo mbovu ambazo hata mtoto mdogo zitampatia uvivu wa kuzisikiliza kwa ubovu wake kisa mtu kahonga au pengine anapewa teke la "ushkaji".Hii ni hali inayouregesha mziki nyuma kwani ni utahira wa hali ya juu kuleta mazao yaliyooza sokoni tukiacha bidhaa nzuri zikiozea shambani.Ile siku DJ na PRESENTERwataweka tamaa kando na kuanzisha harakati za kuupa nafasi mziki mzuri na vipaji halisi hewani,hapo tutakua tumepiga hatua kubwa saana katika safari ya kuufikisha mziki wetu mbali.Kwa mtazamo wangu,upendeleo,ushabiki na "ushkaji" ni saratani kali saana inayoua mziki kwa kasi kubwa na wanaofaa kutibu saratani hii ni ma DJ pamoja na ma PRESENTER.Kivipi? kwanza kabisa kazi mbovu ni mbovu tu iwe imetoka kwa msanii mkubwa au mdogo,kama mtu amechemsha,amechemsha tu na anafaa kurekebishwa tuweke ushabiki kando,pili kuna watu wanaimba tu kisa mjombake au ndugu yake ni DJ au Presenter wa radio flani akijua wazi kwamba atapata shavu la kutoka kimabavu hata kama kipaji sufuri. 
Upendeleo kama huu ukiuweka pembeni itakua tumepiga hatua nyingine kubwa katika safari yetu ya mafanikio.Kwa mara nyingine nasisitiza kuwa pwani hakuna uhaba wa mziki mzuri, hivyo basi hakuna sababu inayopelekea mziki m'bovu kulazimishiwa maskio ya shabiki wakati kuna kazi nyingi nzuri zinazohitaji nafasi katika soko letu la burudani. Tatu,Sioni sababu presenter kuupa asilimia kubwa mziki wa mataifa ya magharibi katika kipindi chake na kuitupa jalalani CD ya msanii wa nyumbani mwenye kipaji ambacho hakitaburudisha tu mashabiki wa nyumbani bali pia kitapandisha uchumi wa sanaa yetu kwa kiwango kikubwa.Ni kwa mara nyingi saana ma presenter mbalimbali wamejitokeza na kukiri kuwa wanalazimika kuucheza mziki wa mataifa ya nnje kwa kisingizio kuwa mashabiki huupendelea saana mziki huo zaidi ya ule wa nyumbani.Huu naweza kusema kuwa ni uongo wa hali ya juu kwani shabiki kwa mara nyingi huzibwa macho na hao ma presenter na kuaminishwa kwa nguvu kuwa wasanii wa nyumbani ni "kanjanja".
Hali hii hupelekea mashabiki kulazimishwa kuamini kuwa kizuri pekee ni kile kigeni.Tunafaa kuelewa kwamba hao wasanii wageni ambao tumewahusudu saana walipewa sapoti na kukubalika kwao kwanza kabla waote mbawa za kuja kuusambaza mziki wao huku kwetu. Hivyo basi tunafaa pia sisi tuondoe nidhamu ya uoga,tujiamini na kile tufanyacho,tujitahidi kwa pamoja ili wasanii hao wageni wakija kwetu kujinadi pia sisi tuwe na vigezo vya kwenda kujinadi huko kwao kwa kuuza kile kizuri tulichonacho.Hii yote italetwa na juhudi za DJ na PRESENTER kuwapa sapoti wasanii bora na sio bora wasanii.Mwiba wa mwisho ni huu hapa.Mtangazaji hafai kujivika maringo mbele ya msanii,anachofaa kutambua ni kuwa sanaa imemsaidia saana katika kazi yake.Utagundua kwamba mziki ni muhimu kwako wewe mtangazaji endapo utavuta taswira ya kipindi cha top ten bila muziki.hivyo basi mtangazaji elewa kuwa asilimia flani ya pato lako liko mikononi mwa msanii.  

MSANII
Sasa hapa ndio shina kuu la sababu ya makala haya lilipo.Kabla tuendelee namnukuu prof jay kwenye wimbo wa mtazamo akisema"sioni sababu za msingi kuomba kwenye mitaa,kama una kipaji iweje ufe na njaa?" ila katika wimbo huo huo pia namnukuu afande selle akisema "hivi ni lazima sote tuwe wasanii,mimi nadhani imetosha wengine tuwe mashabiki".Hii inaonesha wazi kwamba kila mmoja ana haki ya kuwa msanii kwani mziki hauna mwenyewe,ila wasanii ni wengi ila wachache saana ndio wenye vipaji.Talanta ni kitu cha msingi saana ambacho mtu anafaa kukitambua mapema saana katika safari ya maisha yake.Inasikitisha kuona wasanii wengi wenye tungo dhaifu wanalazimisha kitu ambacho ni dhahiri kuwa hawajahesabiwa na mungu kisa ubishoo.Msanii yoyote ambaye yuko kwenye mziki kutafta umaaarufu anafaa kujua kuwa anaishi katika upande usiofaa wa historia.Tunafaa kuelewa kuwa hata uwe na nia kiasi gani kama talanta huna ya kuimba rudi nyumbani ukajifikirie tena ni talanta gani ambayo mwenyezi mungu alikupa,kwani umaarufu ambao unautafuta kwenye mziki unapatikana katika talanta zingine kwani kuna watu dunia hii wamejenga jina na kuishi maisha mazuri kupitia uchoraji na hata kupiga marimba. mwaka juzi kuna msanii kutoka kundi la MAKEKE FAMILY kwa jina RUDIWUU alitoa dis track ambayo ilielekezwa kwa ma presenter inayoitwa HAKI NA USAWA na kuiweka you tube.Kwenye ngoma ile RUDIWUU aliwatusi ma presenter wengi mashuhuri matusi ya nguoni kwa kuwataja majina mmoja baada ya mwingine akidai kuwa wanawanyanyasa wasanii wa nyumbani kwa kutowapa airplay.Kwa mtazamo wangu wimbo ule kama ulikua unawakilisha kilio cha wasanii wa pwani basi ni aibu kubwa saana kwa sanaa ya pwani kuwa na mabalozi kama wale.Kwanza kabisa wimbo ulikua unaitwa "HAKI NA USAWA". Ni haki gani hiyo anayoizungumzia?

 Tunafaa kujua kuwa sio haki ya msanii kuchezwa kwa radio station,ingekua ni haki basi kesi zingekua zimejaa kortini au barabara zingekua haziishi maandamano.Sote tunafaa kuelewa kuwa katika hii safari Producer,msanii,presenter,DJ na shabikitunategemeana.Tunafaa kuelewa kuwa stesheni za runinga na redio vipo kibiashara,kujuza na kuelimisha huku fungu la msanii la kuburudisha likija mwisho kabisa.Mziki na burudani vinatumika tu kama kivutio kwa wasikilizaji.Hii inaonyesha wazi kuwa mmiliki atachagua kinachovutia kwa wasikilizaji wake ili kukidhi mahitaji ya ushindani mkubwa uliopo sasa katika sekta ya burudani na uanahabari.Jukumu lote hili la kuchagua kilicho bora kwa skio la msikilizaji linaanguka kwa mikono ya presenter.

Hivyo basi wewe kama msanii unafaa kuwajibika pia katika harakati zako za kutoa mziki mzuri ambao utakua unamsaidia yule mtangazaji pamoja na DJ kujenga jina kwa yule shabiki wanayemlenga.Kuna msemo unao sema asiyefanya kazi naasile,vilevile msanii ambaye hatajitahidi katika ubunifu hafai kuwa na nafasi katika skio la shabiki.

No comments:

Post a Comment